NA IS-HAKA OMAR, MARA.
CHAMA Cha Mapinduzi
(CCM), kimesema ndani ya miaka 45 kimesimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani
yake iliyoleta maendeleo yenye tija kwa wananchi wa makundi yote.
Hayo ameyaeleza leo Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na
waandishi wa habari juu ya sherehe za maadhimisho ya kilele cha kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika
Mkoani Mara.
Amesema Chama Cha
Mapinduzi kimekuwa ni taasisi imara ya kisiasa barani Afrika kinachowapelekea wananchi
wa Mijini na Vijijini maendeleo endeleovu bila kujali tofauti za kisiasa.
Ameeleza kuwa mnamo
Novemba 5,1976 Mkutano Mkuu wa pamoja wa Halmashauri Kuu za Taifa za vyama vya
TANU na ASP ulifanyika mjini Zanzibar ,uliamua kuvunja vyama hivyo ili kuunda
chama kipya ,Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Amesema vyama hivyo
vya ukombozi vilivunjwa kwa heshima na taadhima kubwa ,si kwa sababu
vilishindwa kutimiza malengo yao,bali ni kwa nia ya kupata chama kimoja
kipya,kilicho imara na madhubuti kukabiliana na changamoto za kudumisha umoja
wa kitaifa na kulera maendeleo ya watu wa Tanzania.
Shaka, amefafanua
kwamba lengo kuu la CCM iliyozaliwa Februari 5, 1977 kutokana na ridhaa ya
wanachama wa vyama viwili, ni kuongoza mapambano magumu ya kudumisha na
kumarisha uhuru wa nchi na Watanzania wote.
Amesema kuwa katika
kipindi cha miaka 45 ya uhai wake, CCM imefanya mengi mazuri kama ilivyokuwa
kwa TANU na ASP, imeendelea kuwaongoza Watanzania sio tu katika kulinda uhuru wa
nchi ya bali pia katika harakati za kujiletea maendeleo, mafanikio
yanayoonekana katika utekelezaji wa sera zake.
Amesema mafanikio
makubwa yaliyofikiwa kwa kipindi hicho ni kudumu na kuimarika kwa Muungano
ambapo changamoto zake zimekuwa zikitatuliwa na hatimaye kuondosha manung’uniko
miongoni na kuongeza upendo na mshikamano kwa Serikali zote mbili.
Shaka, amefafanua
kwamba mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na mfumo madhubuti na imara wa
kisiasa uliojengeka ndani ya CCM.
Amesema ndani ya
kipindi hicho cha miaka 45, Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika
sekta ya miundombinu ya barabara, umeme,afya,elimu,teknolojia,kilimo na uvuvi.
“ CCM ina mengi ya
kujivunia katika kipindi cha miaka 45 toka izaliwe, imefanya mengi makubwa
katika kuimarisha Demokrasia,uchumi,maendeleo na misingi imara ya kiutawala.
Mafanikio hayo
yanatokana na misingi imara ya kisiasa na kiuongozi iliyorithishwa na Vyama vya
ASP na TANU vilivyoacha mazingira rafiki ya kimfumo yanayokifanya Chama kuwa
imara siku zote.”, alisema Shaka.
Katika maelezo yake
Shaka, amesema ndani ya kipindi hicho CCM imekuwa mwalimu wa Demokrasia,sikivu
na kuheshimu uwepo wa vyama vingine vya kisiasa vilivyopo nchini.
Kupitia mkutano huo
Katibu huyo wa NEC, aliyataja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kuwa ni
pamoja na CCM kuwa na mtaji wa kiuchumi wa zaidi ya Shilingi Trioini 1.5.
Ameeleza kwamba
kiwango hicho cha mtaji ni miongoni mwa vigezo mahsusi vinavyotyofautisha CCM
na vyama vingine ya kisiasa nchini na barani Afrika kwani kina uwepo wa
kujiendesha chenyewe kiuchumi na kimapato.
Mafanikio mengine
amesema ni namna CCM kilivyokuwa na mfumo imara wa kuchagua na kuteua viongozi
kwa kufuata kanuni,taratibu na Katiba ya Chama ya mwaka 1977.
Ameongeza kuwa
mafanikio mengine makubwa ni kuimarika kwa Umoja na Mshikamano sambamba na
amani na utulivu ambayo ni matunda yanayowanufaisha wananchi wote bila kujali
tofauti zao za kisiasa.
“ Nchi inapokuwa na
amani wananchi wa makundi yote wanapata fursa pana ya kufanya shughuli zao za
kujiletea maendeleo, kwa sasa kila Mtanzania ana uhuru wa kusafiri na kuishi
popote ndani ya nchi hii bila kusumbuliwa”, alisisitiza
Amesema CCM ina
muundo imara wa kiungozi kuanzia ngazi za mashina hadi Taifa na maamuzi yote
ufanyika kwa kufuata vikao halali, mafanikio hayo hayapo katika chama chochote
cha kisiasa nchini.
Shaka, amesema CCM
inampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti
wake Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2022.
Amesema kasi ya
kiutendaji ya Rais Samia ni kielelezo tosha cha kuonyesha Dunia kuwa Tanzania
ina kiongozi imara,mchapakazi,mzalendo,mbunifu,mtetezi wa haki za makundi yote na kinara wa Diplomasia.
Katibu huyo wa NEC,
amemtaja Rais huyo kuwa ni alama ya ushindi wa kudumu katika uwanja wa
Demokrasia nchini unaotafsiriwa na CCM kuwa ni ushindi uliotukuka katika nyanja
za kisiasa.
Akijibu hoja za
baadhi ya waandishi wa habari, amefafanua kuwa lengo la kufanyika kwa kilele
cha maadhimisho hayo Mkoani Mara ni kumuenzi Rais wa kwanza wa Tanzania hayati
Mwl.Julius Kambarage Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa wa kimaendeleo
alioufanya enzi za uhai wake na kuiheshimisha Tanzania Kiaifa na Kikanda na
Kimataifa.
Akizungumzia
maadhimisho ya kilele cha sherehe hizo amesema CCM inawaalika Wananchi wote wa
Mkoaa wa Mara, Mikoa jirani na Watanzania wote kuhudhuria sherehe hizo
zitakazofanyika Februari 5, 2022 na zitaanza na matembezi ya mshikamano
yatakayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.