SHAKA- MIAKA 45 YA CCM YAVUNJA REKODI, ASEMA SAMIA NI ALAMA YA USHINDI.


NA IS-HAKA OMAR, MARA.




    KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa , Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Sherehe za Maadhimisho ya Kilele cha kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika kesho Mkoani Mara.
(Picha na Is-kaka Omar- Afisi Kuu ya CCM Zanzibar).



NA IS-HAKA OMAR, MARA.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema ndani ya miaka 45 kimesimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani yake iliyoleta maendeleo yenye tija kwa wananchi wa makundi yote.

Hayo ameyaeleza leo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya sherehe za  maadhimisho ya kilele cha kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika Mkoani Mara.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kimekuwa ni taasisi imara ya kisiasa barani Afrika kinachowapelekea wananchi wa Mijini na Vijijini maendeleo endeleovu bila kujali tofauti za kisiasa.

Ameeleza kuwa mnamo Novemba 5,1976 Mkutano Mkuu wa pamoja wa Halmashauri Kuu za Taifa za vyama vya TANU na ASP ulifanyika mjini Zanzibar ,uliamua kuvunja vyama hivyo ili kuunda chama kipya ,Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Amesema vyama hivyo vya ukombozi vilivunjwa kwa heshima na taadhima kubwa ,si kwa sababu vilishindwa kutimiza malengo yao,bali ni kwa nia ya kupata chama kimoja kipya,kilicho imara na madhubuti kukabiliana na changamoto za kudumisha umoja wa kitaifa na kulera maendeleo ya watu wa Tanzania.

Shaka, amefafanua kwamba lengo kuu la CCM iliyozaliwa Februari 5, 1977 kutokana na ridhaa ya wanachama wa vyama viwili, ni kuongoza mapambano magumu ya kudumisha na kumarisha uhuru wa nchi na Watanzania wote.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 45 ya uhai wake, CCM imefanya mengi mazuri kama ilivyokuwa kwa TANU na ASP, imeendelea kuwaongoza Watanzania sio tu katika kulinda uhuru wa nchi ya bali pia katika harakati za kujiletea maendeleo, mafanikio yanayoonekana katika utekelezaji wa sera zake.

Amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa kwa kipindi hicho ni kudumu na kuimarika kwa Muungano ambapo changamoto zake zimekuwa zikitatuliwa na hatimaye kuondosha manung’uniko miongoni na kuongeza upendo na mshikamano kwa Serikali zote mbili.

Shaka, amefafanua kwamba mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na mfumo madhubuti na imara wa kisiasa uliojengeka ndani ya CCM.

Amesema ndani ya kipindi hicho cha miaka 45, Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta ya miundombinu ya barabara, umeme,afya,elimu,teknolojia,kilimo na uvuvi.

“ CCM ina mengi ya kujivunia katika kipindi cha miaka 45 toka izaliwe, imefanya mengi makubwa katika kuimarisha Demokrasia,uchumi,maendeleo na misingi imara ya kiutawala.

Mafanikio hayo yanatokana na misingi imara ya kisiasa na kiuongozi iliyorithishwa na Vyama vya ASP na TANU vilivyoacha mazingira rafiki ya kimfumo yanayokifanya Chama kuwa imara siku zote.”, alisema Shaka.

Katika maelezo yake Shaka, amesema ndani ya kipindi hicho CCM imekuwa mwalimu wa Demokrasia,sikivu na kuheshimu uwepo wa vyama vingine vya kisiasa vilivyopo nchini.

Kupitia mkutano huo Katibu huyo wa NEC, aliyataja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kuwa ni pamoja na CCM kuwa na mtaji wa kiuchumi wa zaidi ya Shilingi Trioini 1.5.

Ameeleza kwamba kiwango hicho cha mtaji ni miongoni mwa vigezo mahsusi vinavyotyofautisha CCM na vyama vingine ya kisiasa nchini na barani Afrika kwani kina uwepo wa kujiendesha chenyewe kiuchumi na kimapato.

Mafanikio mengine amesema ni namna CCM kilivyokuwa na mfumo imara wa kuchagua na kuteua viongozi kwa kufuata kanuni,taratibu na Katiba ya Chama ya mwaka 1977.

Ameongeza kuwa mafanikio mengine makubwa ni kuimarika kwa Umoja na Mshikamano sambamba na amani na utulivu ambayo ni matunda yanayowanufaisha wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa.

“ Nchi inapokuwa na amani wananchi wa makundi yote wanapata fursa pana ya kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo, kwa sasa kila Mtanzania ana uhuru wa kusafiri na kuishi popote ndani ya nchi hii bila kusumbuliwa”, alisisitiza

Amesema CCM ina muundo imara wa kiungozi kuanzia ngazi za mashina hadi Taifa na maamuzi yote ufanyika kwa kufuata vikao halali, mafanikio hayo hayapo katika chama chochote cha kisiasa nchini.

Shaka, amesema CCM inampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wake Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2022.

Amesema kasi ya kiutendaji ya Rais Samia ni kielelezo tosha cha kuonyesha Dunia kuwa Tanzania ina kiongozi imara,mchapakazi,mzalendo,mbunifu,mtetezi wa haki za makundi yote  na kinara wa Diplomasia.

Katibu huyo wa NEC, amemtaja Rais huyo kuwa ni alama ya ushindi wa kudumu katika uwanja wa Demokrasia nchini unaotafsiriwa na CCM kuwa ni ushindi uliotukuka katika nyanja za kisiasa.

Akijibu hoja za baadhi ya waandishi wa habari, amefafanua kuwa lengo la kufanyika kwa kilele cha maadhimisho hayo Mkoani Mara ni kumuenzi Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa wa kimaendeleo alioufanya enzi za uhai wake na kuiheshimisha Tanzania Kiaifa na Kikanda na Kimataifa.

Akizungumzia maadhimisho ya kilele cha sherehe hizo amesema CCM inawaalika Wananchi wote wa Mkoaa wa Mara, Mikoa jirani na Watanzania wote kuhudhuria sherehe hizo zitakazofanyika Februari 5, 2022 na zitaanza na matembezi ya mshikamano yatakayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.



 

 

 

   

No comments:

Post a Comment