VIONGOZI MBALIMBALI WAUZULIA KATIKA DUA YA KUMBUENZI ARIEKUWA RAIS WA KWANZA WA ZANZIBAR HAYATI ABEID AMANI KARUME

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi,jana amewaongoza mamia wa wananchi visiwani hapa katika dua maalum ya kumuombea mzee Hayati Abeid Amani Karume ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 49 ya kifo chake tangua alipouwawa Aprili 7 mwaka 1972.


Mbali na Rais Dk.Mwinyi pia kwa upande wa wanawake katika dua hiyo Rais wa awamu ya nane ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani aliwaongoza wanawake kwenye dua hiyo iliofanyika ofisi kuu za Chama Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar.  






Baada ya kumalizika kwa dua hiyo Rais Dk.Mwinyi alianza  kuweka shada ya maua katika kaburi la mzee Karume,akifuatiwa na Rais Samia kuweka pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Venance Mabeyo na mtoto wa mzee Karume Ali Abeid Amani Karume akiwakilisha kwa niaba ya familia.




Akitoa nasaha katika dua hiyo Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Khalid Mfaume alisema mzee Abeid Amani Karume ataendelea kukumbukwa toka alipofariki mwaka 1972 kutokana na kutandika misingi imara ya waafrika kujitawala wenyewe,kuimarisha umoja mshikamano na kupendana.

Alisema mzee Karume aliacha hadithi nzuri kwa watanzania hasa wananchi wa Zanzibar ambayo inaendelea kukumbukwa milele.

 "Naomba ninukuu msemo wa Rais wetu wa awamu ya pili mzee Ali Hassan Mwinyi ambao mara nyingi anapenda kusema kuwa maisha ya mwanaadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa na ndio maana leo tunaendelea kumkumbuka jemedari wetu kwa mambo mazuri aliyotuachia," alinukuu 





Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo alisema jana ni kumbukumbu ya miaka 49 ya kifo cha Hayati Mzee Karume na kwamba ni kiongozi ambaye maneno na maono yake bado yanaishi mpaka leo.

Alisema hotuba za Hayati Mzee Karume toka miaka hiyo iliyopita lakini ni kama jambo alilolizungumza leo au jana, na kwamba Mzee Karume alikuwa ni kiongozi mwenye maono makubwa sana.

Jafo alisema wakati yeye na baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere walipoasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lilikuwa ni jambo jema sana kwa watanzania.

"Ikiwa leo ni siku ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 49 ya kifo chake sisi watanzania tuna kila sababu ya kuuenzi na kuudumisha muungano huu ambao viongozi wetu hawa wameuasisi," alisema 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud alisema, uongozi wa Hayati Mzee Karume ni uongozi ambao uliacha alama na ni uongozi amao hautaweza kusahaulika kwa vizazi na vizazi.

Akiyataja mambo mawili makubwa yaliyofanywa na hayati Mzee Karume enzi za uhai wake alisema, jambo la kwanza ni kulikomboa taifa la Zanzibar lakini jambo la pili ni kuletea maendeleo baada ya ukombozi.

Mkuu wa mkoa huyo alisema, mambo hayo makubwa mawili ndiyo yanayomfanya akumbukwe kila wakati na kuendelea kukumbukwa na vizazi vijavyo.

Alisema katika kutekeleza hayo, Mzee Karume alizingatia sana hali za wanyonge na kwamba alitamani wananchi wote wawe sawa kwa kadri ya uwezo wake.

"Kwa hiyo uongozi wake ni wa mfano na ungefaa kuigwa na kila kiongozi katika hili, nikitazama mwenendo wa awamu ya nane katika muelekeo wake unanipa matumaini makubwa ya kuakisi muelekeo wa Hayati Mzee Karume," alisema.

Alisema serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na DK. Hussein Ali Mwinyi imeanza katika kipindi kifupi sana lakini malengo yake na awamu zilizopita yanaakisi muelekeo na mtazamo wa awamu ya kwanza ya Zanzibar.

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema anapokumbukwa Hayati Mzee Karume basia anakumbukwa mtu muhimu sana Tanzania na kwamba ni kiongozi ambaye ni jasiri na jemedari.

Alisema hayati mzee Karume alihakikisha kila mzanzibar anakuwa na uhuru wake tosha, anasimama kama mzanzibar katika uhuru wake na kila kitu chake bila ya kutegemea kutawaliwa na watu wa nje.

Katika maelezo yake alisema wazanzibar na watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kumuombea kwa sababu Hayati Mzee Karume alikuwa na malengo yaliyokuwa yanaendana na matakwa na matarajio ya wazanzibar.

"Leo tunashuhudia maendeleo na fikra zake na kwamba waliomfata wote wameendelea kuzifuata fikra zake na leo tunaona maendeleo makubwa ambayo Zanzibar imeyapiga," alisema

Alisema ukiangalia mwenendo na sera ambazo Dk.Hussein Ali Mwinyi anaenda nazo za kuleta umoja kwa wazanzibar kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa hayo ndiyo ilikuwa dhamira hasa ya Hayati Mzee Karume ya kuwafanya wazanzibar na watanzania kwa ujumla kuwa kitu kimoja.

Naye Katibu wa Idara ya Oganazetion ya CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema mzee Abeid Amani karume anakumbukwa kwa mambo matatu ya msingi ikiwemo kutoa heka tatu kwa wananchi ili waweze kulima kwa ajili ya kujipatia riziki.

 Alisema jambo jingine atakaloendelea kukumbukwa kiongozi huyo ni kuifanya elimu bure ili kuona kila mtoto mwenye haki ya kusoma basi anasoma bila ya malipo na kutoa matibabu bure.

 Pia,alisema marehemu mzee Abeid Amani Karume amejenga misingi ambayo haitoweza kusahaulika kwa vizazi vya sasa na vitakavyokuja.

 Alisema Mzee Abeid Amani Karume aliimiza umoja mshikamano na upendo kwa wazanzibari ambapo matakwa hayo yanaendelea kuendelezwa na viongozi wa serikali.                

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Sadala (Mabodi) alisema miaka 49 ya kifo cha hayati mzee Abeid Amani Karume ni elimu tosha kwa wananchi kuyaendeleza yale yote aliyoyaacha jemedari huyo hasa suala la amani umoja na mshikamano.

Pia alisema jambo jengine ni kubadilika katika siasa za kujitegemea ambapo mzee Karume alionyesha hayo na kuunda miundombinu endelevu yenye kudumu. 

Hata hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kudumisha Mapinduzi ambayo ndio historia kubwa katika nchi yao na kutunza hazina ya nchi yao ikiwemo wazee na hazina ya nchi ikiwemo maendeleo, watu na umoja wao katika kufanya kazi na kujituma ambayo ndio nguzo kuu aliyoiacha marehemu Karume.

 Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohammed alisema Zanzibar imekuwa ikiendeleza muono wa hayati Abeid Amani Karume na kujivunia kuendelea umoja, amani na mshikamano.

Alisema ni imani kwamba yale yote aliyoyaacha yanaendelea kuendelezwa na viongozi wakuu wa serikali kuanzia awamu ya pili hadi awamu ya nane iliyokuwepo madarakani.

Dk.Khalid alisema hivi sasa nchi imepiga hatua kubwa za kimaendeleo hasa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kwamba  alama zote zilizoachwa na hayati mzee Abeid Amani Karume tokea mwaka 1972 zinaendelezwa mpaka leo ikiwemo alama ya elimu bure ambayo inatolewa bila ya ubaguzi, matibabu bure, makazi bora, kuwatunza wazee na watoto yatima. 

Viongozi mbalimbali walihudhuria katika dua hiyo akiwemo

Mkuu wa Majeshi,Ulinzi na Usalama Venance Mabeyo,Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othaman Masoud Othman,Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah,Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar,Dk.Abdulla Juma Sadalla. 

Wengine waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi,Rais mstaafu wa awamu ya sita ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Amani Abeid Karume,Rais mstaafu wa awamu ya saba ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

Mbali na hao wengine ni Makamu wa Rais mstaafu wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.Ghalib Bilal,Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd,Mke wa hayati Abeid Amani Karume mama Fatuma Karume, 


No comments:

Post a Comment