RAIS WA ZAMZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZIDK.HUSSEIN MWINYI AWATAKA WANANCHI KUFANYA MAZOWEZI ILI KUWEKA KINGA NA KUDHIBITI MAGONJWA MWILINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kufanya mazoezi kwa lengo la kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa huko uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mazoezi ya Viungo Kitaifa yaliyoanzia kiwanja cha Mapinduzi Square Michenzani na kuishia Uwanja wa Amaan ambapo Rais Dk. Hussein Mwinyi alishiriki kikamilifu pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkewe Mama Mariam Mwinyi.

Viongozi wengine walioshiriki ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla pamoja na Mkewe Mama Sharifa, Spika wa Baraza na Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mkuu wa Mkoa Idrisa Mustafa Kitwana, Mawaziri, vikundi vya mazoezi pamoja na wananchi.

Alisema kuwa mazoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua kwani kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angau tatu kwa wiki na kumfanya mtu kutoka jasho.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka wananchi hasa wale wanaofanya kazi maofisini kuongeza bidii ya kufanya mazoezi na wale wanaotumia magari wanapaswa kupanga shughuli ambazo zitawafanya kila siku watembee kwa miguu.

Kwa upande wa waajiri aliwashauri kuimarisha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wao wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi hata katika sehemu zao za kazi kwa kuanzisha timu za michezo pamoja na kutenga siku maalum katika mwezi kwa ajili ya mabonanza ya michezo.

Alisisitiza kuwa Mazingira rafiki ya kufanya mazoezi kazini ni kutenga  vyumba vya mazoezi na kununua vifaa vya michezo hatua ambayo itaimarisha afya ya watumishi na kupunguza kharama za matibabu katika taasisi husika.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ili kufanya mazoezi kuwa endelevu Maofisa Michezo wa Mikoa na Wilaya wanawajibu wa kuongeza uhamasishaji na uundaji wa vikundi vya mazoezi vya pamoja katika maeneo yao.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Ardhi na Makaazi zina mamlaka ya kusimamia na kuweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi.

Dk. Mwinyi alisema kuwa Matamasha ya michezo na utamaduni yanatakiwa kuwa kichocheo cha kushirikisha vitu vingi ikiwemo michezo ya jadi na mashirndano ya basikeli katika maeneo mbali mbali ambayo yana mchango mkubwa katika  kutunza afya za washiriki wa michezo hiyo.

Alisema kuwa katika matamasha hayo ni vyema wananchi wakahamasishwa kupima afya zao ili kuongeza hamasa ya wananchi huku upimaji huo ni vyema ukawa bure.

Aidha, alisema kuwa bonanza hilo linapelekea watu kujuana na kubadilishana mawazo huku akieleza dhamira ya wazi ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimaisha michezo ikiwemo Bonanza la Michezo na vikundi vya mazoezi linalofanywa kila tarehe mosi ya Januari ya kila mwaka.

Pia, alieleza azma ya Serikali ya kuhamaisha michezo ya asili ya Zanbzibar ikiwemo mashindano ya resi za ngalawa, bao, karata, mchezo wa ngombe na mengineyo ambapo pia, watu wenye ulemavu watahamasishwa na kupatiwa vifaa.

Alisema kuwa michezo ni nyenzo madhubuti katika kulinda avya za wanaadamu na kuwajengea uimara na ustahamilivu ambapo Sera ya michezo inatambua umuhimu wa michezo ikiwemo kuhamasisha uma wa Wazanzibari kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo.

Aliongeza kuwa Serikali itawezesha kupatikana viwanja na michezo na vifaa vya michezo vilivyobora na vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya mic hezo nchini.

Katika Tamasha hilo, Rais Dk. Mwinyi alitoa vyeti maalum kwa washiriki wa Tamasha hilo kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara ambapo mapema wanamazoezi hao walipita mbele ya jukwa kuu alilokaa Rais huku wakionesha umahiri wao wa mazoezi.

Sambamba na hayo Wanamazoezi hao walionesha namna ya ufanya wa mazoezi wakiongozwa na walimu wao mahiri wa mazoezi ambapo walionesha ufundi na hamasa kubwa ya ufanyaji wa mazoezi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan King jumla ya vikundi 97  vimeshiriki katika Bonanza hilo  vikiwemo 60 kutoka Unguja, 20 kutoka Pemba na 17 kutoka Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment