DK. SHEIN ATOA SOMO LA MAPINDUZI

 NA  IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR

 

MAKAMU wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk.Ali Mohamed Shein  amesema Wananchi walifanya Mapinduzi ya januari 12, mwaka 1964 kutokana na kunyimwa haki za msingi zikiwemo huduma muhimu za kijamii,kiuchumi na kutopata uhuru wa kujitawala wenyewe.

Akizungumza na makatibu wa matawi ya chama kutoka wilaya za Ilala ,Temeke ya Mkoa wa Dar es Saalam ofisini kwake Kisiwandui mjini Unguja walipomtembelaea Ofisini kwake Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Alisema  sababu ya kutokea kwa mapinduzi hayo ni unyonge waliokuwa nao wanzanzibar ambapo walikuwa wanyonge sana kutokana na kuwa hakuwa na haki yeyote hawezi kumiriki ardhi kwa ajili ya kulima hata kujenga nyumba.

Makamu huyo Mwenyekiti alisema pia wanzanzibar walikuwa hawana haki ya kupata elimu zaidi ya watoto wa kizungu,wahindi na waarabu ndio waliokuwa wakipata elimu.

"Hakuna mwananchi aliyetibiwa hospitali wengi walifukuzwa na kukoseshwa haki hiyo ya kupata matibabu,"alisema

Makamu Mwenyekiti huyo alisema mapinduzi ndio uhai wa wanzanzibar kutokana na kuwa ndio yamewakomboa na kwamba kusingefanyika mapinduzi hayo wafanyakazi wanzanzibar na wakulima wangekuwa bado wapo katika ukoloni mpaka leo.

"Mwaka 1964 hadi leo ni miaka 57 sisi wengine vugu vugu la kisiasa tumeliona mimi uchaguzi wa mwanzo 1957 nimeuona lakini sikufanikiwa kupiga kura maana nilikuwa nipo darasa la kwanza

wazee wanakwenda kupiga kura ninawaona ninauliza kuna nini wananiambia kuna uchaguzi lakini wanawake hawakupiga kura mnaweza kuona kazi iliokuwepo ukoloni huo,"alisema

 

Alisema uchaguzi huo ASP ilishinda kwa viti vitano kati ya viti sita vya Zanzibar ahadi ikatolewa kuwa atakayeshinda uchaguzi atapewa uhuru lakini ASP haikupewa uhuru licha ya kushinda huku kiti hicho kimoja kilikuwa ni cha mtu binafsi kati ya viti hivyo kutoka chama cha jumuiya ya wahindi na kwamba hakuna chama cha upinzani kilichokishinda ASP.

"Wazee wetu wakaambiwa mpira umekwisha uchaguzi mwingine utafanyika mwaka 1961 aandaeni mazingira ya kushindana kisiasa ninachotaka kuwaambia ni kuwa ASP ni chama kilichoundwa na jumuiya mbili kubwa jumuiya ya African Association na jumuiya ya Shiraz jumuiya hizo mbili zikaungana ndipo mwaka 1957 kizaliwa ASP,"alisema Dk.Shein

Alisema baada ya hapo ASP ikaingia uchaguzi wa vyama vingi kipindi cha Januari mwaka 1961 kikashinda tena ikapata viti tisa kati ya viti 22 chama cha ZPP kilipata viti vitatu na Hizbu kilipata viti nane.

"Mzee Karume akaambiwa aunde serikali lakini aliaambiwa hajapata idadi kubwa ya viti lakini ilishindikana akaitwa kiongozi wa Hizbu naye akaambiwa akaunde serikali naye akashindwa kutokana na kuwa kati ya viti vitatu vya ZPP kimoja kilipelekwa ASP na viwili vilipelekwa Hizbu na hatimaye ikiwa idadi zinafanana viti 10 kwa 10,"alisema

 "Lakini kura zetu za ASP zilikuwa nyingi zaidi ya asilimia 60 ikaamuliwa kuundwa kwa serikali ya mseto mzee Karume alichaguliwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na kiongozi wa Hizbu akachaguliwa kuwa Waziri wa Elimu na Habari na Mohamed Shamte wa ZPP akaingizwa kupewa Wizara ya Ardhi ikabidi uchaguzi urudiwe tena Juni mwaka 1961 baada ya miezi mitano lakini ASP ilishinda mara mbili hadi hapo,"alisema

Alisema kabla ya kufanyika kwa uchaguzi akaja mtu kutoka Uingereza ambaye ni mtaalamu wa kukata majimbo katika nchi za jumuiya za  madola akayakata majimbo kutoka majimbo 22 na kufanya ASP kushindwa kwa majimbo licha ya kuwa kura bado kuwa nyingi.

"Majimbo yenye wakazi wengi wa ASP yakawa yamekatwa pakubwa wakazi wa Hizbu yakawa yamekatwa kidogo na mfano upo jimbo la Malindi kulikuwa na wakazi wasiofika 900 likawa jimbo moja aliyeshinda kapata kura 538 jimbo la Mkunazini wakazi wake walikuwa hawafiki

800 aliyeshinda alikuwa ana kura 400 jimbo la Kwahani la Mzee Karume lina wakazi 5000, jimbo la Mwembe Radu lina watu 4000 hivyo tukashindwa kupata idadi kubwa ya majimbo hivyo ASP haikupewa uhuru mara ya tatu,"alisema

Alisema baada ya hapo uchaguzi mwingine ukaitishwa wakisema kuwa ndio uchaguzi wa mwisho Julai mosi mwaka 1963 wakati huo akiwa anasoma sekondari ambapo ASP ikashindwa kwa kupata majimbo 13 vyama vingine viwili vikaungana na kuwa majimbo 18 ambapo ZPP ikapata majimbo matatu Hizbu ikapata majimbo 15 lakini bado kura za ASP zikiwa na asilimia nyingi.

"Hayo ndio uonevu wenyewe kabla ya uchaguzi wazee wetu wakaenda Uingereza walienda  kutunga katiba ya Zanzibar sasa ile katiba ndio iliomuuzi mzee Karume akasema katiba hii inatungwa Zanzibar kiongozi wake atakuwa Sultan wakati sisi tunataka uhuru aondoke waingereza wanasema atabakia kuwa kiongozi wenu akataka kutoka nje ya mazungumzo wazee wenzake  wakamuomba abaki na kilichomuuzi ni Zanzibar kuwa itaitwa dola ya Sultan,"alisema

Alisema wazee wakakubali wapewe uhuru wao ambao ASP walikuwa wanauita uhuru wa  karafuu na sherehe zao za uhuru zikafanyika maisara ambapo alikuja mumewe Malikia wa Uingereza kukabidhi uhuru kwa Sultan.

"Katika sehemu ya kuhutubia pale palikuwepo kiongozi wa Hizbu,kiongozi wa ZPP ambaye  alipewa nafasi ya Waziri Kiongozi lakini hakuwepo kiongozi yeyote wa ASP wanachama wamejiinamia basi uhuru ukatolewa 10 Desemba mwaka 1963 sisi tukasema si uhuru wetu uhuru wenu nyinyi,"alisema

Alisema ASP ikaona hakuna njia nyingine ya kuiondoa serikali zaidi ya Mapinduzi ikasubiria utawala wa Uingereza aondoke mnamo 12 Januari mwaka 1964 na hadi leo miaka 57 wanzanzibar wamejitawala wenyewe na kwamba nchi hii mnyonge alikuwa hana ardhi ya kulima,kujenga na hapati hata elimu.

Dk.Shein alisema vijana wa sasa wanatakiwa kuendeleza mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi wa zamani ili kupata maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) tawi la Saba Saba, Hasma Othaman Mpanda alisema baada ya kupata somo hilo la mapinduzi alilolitoa Dk.Shein amejifunza mambo mengi ambayo alikuwa hayafahamu.

"Leo nimejifunza mambo mengi ambayo nilikuwa siyajuhi nimeyajua hivyo nitayabeba kwa ajili ya kuwafundisha wenzangu huko Dar es Saalam kuhusu mapinduzi mfano alisema kipindi cha zamani wazee wetu walikuwa wakipigania uhuru dhidi ya vibaraka wa Sultan kwa kweli nimejifunza vitu vipya kwa upande wangu,"alisema

Alisema vijana na wanachama wa CCM kwa ujumla wanatakiwa kujifunza historia hali ya Zanzibar ili kupata ukakamavu na uzalendo usioyumba.

Aliahidi kwamba darasa alilotoa Dk.Shein juu ya sababu za kufanyika Mapinduzi ya Zanzibar na yeye atahakikisha anawafundisha Wana CCM na makada wengine ili elimu hiyo iendelee kuishi katika fikra za makada hao.


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, akizungumza na makatibu wa matawi ya CCM ya Ilala na Temeke Dar es saalam waliomtembelea Ofisi kwake Kisiwandui Zanzibar.



BAADHI ya Makatibu hao wakifuatilia nasaha zinazotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Ofisini kwake Kisiwandui Zanzibar.


MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mwalimu Kombo Hassan Juma  akizungumza na wageni hao kabla ya kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, azungumze katika hafla hiyo.


No comments:

Post a Comment