MASHEHA,MADIWANI WATAKIWA KUFICHUA MIRADI MISIOTEKELEZWA

 

Masheha na Madiwani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja, wametakwa kufichua miradi isiyotekelezwa katika mamlaka husika ili kuchukuliwa hatua za kuleta maslahi kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alitoa kauli hiyo Mkokotoni alipokuwa akizungumza na Masheha, Madiwani na Viongozi wengine wa mkoa huo katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kaskazini, Unguja.

Alisema viongozi hao wana dhamana na msaada mkubwa wa kutanabahisha maeneo hayo kwani ndio wanaojua watu wanaovamia au wanaojenga katika maeneo bila ya kibali hivyo hawapaswi kulifumbia macho suala hilo.

“Kuna miradi mingi lliyoanzishwa lakini mwisho wa siku haiendelei badala yake watu wanakula pesa za serikali bila ya kujali athari zinazoweza kujitokeza kwa jamii,” alieleza Masoud.

Aidha, aliwatoa hofu viongozi hao na kuwataka kusimamia ipasavyo maeneo hayo na kuwasaidia wananchi na kujua changamoto zao bila ya kuonea mtu aibu wala muhali kwani zama hizo hivi sasa zimepitwa na wakati.

“Wakati umefika kwa nyinyi viongozi kufichua miradi ambayo inaweza kuleta tija kwa jamii na taifa sambamba, mkifanya hivyo itakuwa mnaisaidia serikali kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, uzembe na ubabaishaji,” alieleza Masoud.

Aidha Masoud aliwaagiza watendaji wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) ili kuhakikisha upotevu na ubadhirifu unakwisha ndani ya mkoa huo.

Mapema mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘B’, Rajab Ali Rajab, alisema uchaguzi umemalizika kwa amani na usalama wilayani humo na kilichobaki ni kugawana majukumu na kufanyakazi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kulijenga taifa kwa maslahi ya nchi.

Nao watendaji wa mkoa huo walimshukuru waziri huyo kwa kuwapatia muongozo wa utekelezaji kwa ufanisi majukumu yao na kuahidi mapungufu na changamoto zilizopo kuzifanyia kazi kwa ufanisi zaidi. 

No comments:

Post a Comment