DK.MWINYI: AAHIDI KUTEKELEZA AHADI YAKE YA KUPAMBANA NA RUSWA NA WABADHIRIFU WA MALI ZA UMMA

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kupambana na rushwa, ubadhilifu wa mali ya umma na uzembe katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambacho hivi sasa anakiongoza rasmin.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika sherehe za mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), mara baada ya kutawazwa rasmin kuwa Mkuu wa Chuo hicho, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein, ndani ya kampasi ya Chuo hicho huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja. Hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo, atafuatilia kwa karibu makusanyo ya ada, ruzuku kutoka Serikalini na kwa wahisani, matumizi ya thamani ya vitu vinavyonunuliwa pamoja na vianzio mbali mbali.

Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Chuo hicho kusimamia vizuri na kwa umakini na uadilifu rasilimali za chuo, watunze vizuri nyaraka mbali mbali zenye kuonesha mali zinazomilikiwa na chuo zikiwemo hati miliki za ardhi, nyumba na majengo mengineyo huku akihiza haja ya kufanyiwa matengenezo nyumba na majengo ya chuo na nyumba zote zinakaliwa wakati wote.

Aliwataka wahadhiri na wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na nidhamu kwa kuzingatia sheria na maadili yanayoongoza kazi zao pamoja na kujiandaa kitaaluma ili wawe wanapanda daraja kwa kulingana na taratibu zilizopo.

Alisisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira na kuutaka uongozi kuhakikisha unaweka mazingira katika Kampasi zao ili yaweze kuvutia kwa kuwa na miti ya vivuvi na bustani huku akiwataka kujiandaa kwani hivi karibuni atafanya ziara katika Kampasi zote kuangalia hayo yote aliyoyasema.

Aidha, Rais Dk. Hussein mwinyi alisema kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein ameonesha njia kwamba Chuo hicho ni miliki ya Watu wa Zanzibar na kinaendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hivyo ni lazima kifundishe masomo yanayoendana na mahitaji ya wananchi kiuchumi na kijamii.


Kwa msingi huo Rais Dk. Mwinyi aliitaka (SUZA) kuwa mfano wa Chuo chenye mitaala na programu mbali mbali za ufundishaji zinazozingatia mahitaji ya nchi pamoja na sera na mipango ya maendeleo ya muda mfupi, muda wakati na muda mrefu.

Alieleza kuwa (SUZA) ina kazi kubwa ya kufundisha wataalamu wa kutosha wanaohitajika kusimamia uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Mstaafu Dk. Shein kwa kumkabidhi Chuo kikiwa kimepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka 10 cha uongozi wake ambapo miundombinu imeimarika, idadi ya Kampasi na idadi ya wanafunzi imeongezeka, wahadhiri na wafanyakazi pamoja na programu zinazofundishwa na hadhi na sifa ya elimu inayotolewa imekuwa.

Rais Dk. Hussein ameitaka (SUZA) kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa kufanya tafiti na kuweka mkazo wa matumizi ya tafiti katika maeneo mbali mbali yanayohusu uchumi wa Buluu na sekta nyengine za uchumi.

Alieleza kuwa ni kazi ya (SUZA) kwa kushirikiana na taasisi nyengine za Elimu ya Juu ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kufanya tathmini ya tafiti zilizofanywa ndani ya kipindi cha 2015-2020 na uhalisia wa tafiti hizo kwa mahitaji ya nchi.

Hivyo, alieleza kuwa Zanzibar ina haja ya kuwa na ajenda mpya ya utafiti wa Kitaifa na kusisitiza kuachana na tabia ya kutegemea wahisani hata katia mambo muhimu ya maendeleo wanayoweza kufanywa na Wazanzibari wenyewe.


RAISA  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempa shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba, Rais Mstaafu wa Zanzibar awamu ya saba  Dk. Ali Mohamed Shein.


Katika hafla hiyo, Rais Dk. mwinyi aliwatunuku wanafunzi 244 wa ngazi ya Cheti, 799 kwa ngazi ya Stashahada, 453 kwa ngazi ya Shahada na 28 kwa ngazi ya Uzamili huku akiwakabidhi vyeti na zawadi wanafunzi bora watatu akiwemo Nassra Suleiman Mohammed wa Shahada ya Kwanza aliyepata GPA 4.9, Ali Abdalla Moh’d wa Stashahada aliyepata GPA 5.0 na Hanafi Abdallah Moh’d aliyepata GPA 4.9

No comments:

Post a Comment